JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi

BITEKO AWAFUNDA WATAALAM WA UNUZI NA UGAVI, ATAKA MABADILIKO SEKTA ZA UMMA
22 Apr, 2025
BITEKO AWAFUNDA WATAALAM WA UNUZI NA UGAVI, ATAKA MABADILIKO SEKTA ZA UMMA

Naibu Waziri Mkuu na  Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka wataalam wa ununuzi na ugavi nchini kizingatia misingi ya maadili ya taaluma yao ili kuiwezesha Serikali kuleta maendeleo kwa wananchi wake.

Dkt. Biteko amesema hayo wakati akifungua Kongamano la 15 la Wataalam wa Ununuzi na Ugavi linaloendelea Jijini Arusha. 

Amesema wataalam wa ununuzi na ugavi ni muhimu katika kuchagiza maendeleo na Serikali inawategemea ili kufanikisha mipango yake. 

“ Wataalam wa manunuzi na ugavi mna mchango mkubwa, zaidi ya asilimia 70 ya bajeti nzima ni kwa ajili ya manunuzi, hivyo kuweni waadilifu, Chukieni Rushwa na kushauri namna bora ya kufanikisha mipango ya Maendeleo” amesema Dkt. Biteko.

Amesema kutokana na ukubwa wa majukumu yao kuna uwezekano rushwa kubwa ikapita mikononi mwao, hivyo majadiliano haya yawawezeshe kuzuia na kukabiliana na vitendo hivyo. Aidha Dkt. Biteko amesema ni wajibu wa wataalam kujisimamia na kulinda taaluma yao kwa wivu mkubwa ili taaluma hiyo isiingiliwe na watu wasiokuwa na sifa zinazohitajika huku akizitaka mamlaka husika kuwatambua na kuwamotisha wataalam wenye sifa kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, Dkt. Biteko amewataka washiriki wa Kongamano hilo kujifanyia tathimini kuhusu utendaji wao wa kazi ili kuondokana na Changamoto zinazoweza kuichafua taaluma ya ununuzi na ugavi.

“ Zipo sauti nanyi mnazisikia, ili uweze kupata tenda lazima kuwa na urafiki na Afisa ununuzi, wanasema ukifuata taratibu za ununuzi gharama zinaongezeka zaidi ya kawaida, wengine wanasema siri za tenda zinapatikana miongoni mwa watumishi, wengine wanalaumu na wengine wanasifia, Jambo la msingi sikilizeni sauti za watu na mjitathimini,” amesisitiza

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Chande amewataka washiriki kufanya kazi zao kwa kushirikiana huku Wizara yake ikiendelea kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili wataalam wa ununuzi na ugavi.

Amesema miongoni mwa mambo yanayosababisha mkwamo Serikalini ni pamoja na Wivu, choyo na fitna miongoni mwa watumishi, hivyo amewataka kuondokana na mambo hayo ili kukua na kujiletea maendeleo.

“Sheria ya ununuzi wa umma sura 410 inawalinda wataalam wa ununuzi na ugavi hivyo watembee kifua mbele na kuhakikisha wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria zilizopo”.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) Benezeth Ruta ameishukuru Serikali kwa kutenga fedha zinazoiwezesha taaluma hiyo kusonga mbele.