JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi

SERIKALI YAAGIZA WAAJIRI KUWEZESHA WATAALAM UNUNUZI NA UGAVI KUPATA MAFUNZO
05 Jan, 2026
SERIKALI YAAGIZA WAAJIRI KUWEZESHA WATAALAM UNUNUZI NA UGAVI KUPATA MAFUNZO

 

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Musham Ali Munde amewaagiza Waajiri wote nchini kuwawezesha watalaam wa ununuzi na ugavi kupata mafunzo na kushiriki makongamano muhimu yanayohusu taaluma zao ili kuongeza ujuzi, kubadilishana uzoefu wa kitalaam na kiutendaji.

Ametoa agizo hilo leo Desemba 19, 2025 jijini Arusha wakati akimuwakilisha Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar katika ufunguzi wa Kongamano la 16 la Mwaka la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi, linalofanyika kwa siku tatu (03) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).

Naibu Waziri amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuhimiza maendeleo ya rasilimali watu kwa kukuza ujuzi wa kitaaluma na uongozi bora kwa lengo la kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

"Ili kuweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Serikali kupitia bajeti yake ya mwaka huu wa fedha imeelekeza shughuli zote za ununuzi zifanyike katika mfumo wa ununuzi wa kidijitali yaani (NeST) lengo likiwa ni kupunguza gharama za ununuzi, kuongeza kasi ya utekelezaji kuzingatia bei ya soko na hivyo kuleta tija iliyokusudiwa kwa Taifa", amesema Mhe. Munde.

Ameongeza kuwa, serikali haitasita kuchukua hatua ili kurekebisha kasoro yoyote itakayoonekana kukwamisha utekelezaji wa maelekezo husika ikiwa ni pamoja na Serikali kuwa tayari kurekebisha maeneo ambayo yanakwamisha utekelezaji wa maelekezo husika.

Kongamano hilo linawakutanisha wataalam kutoka sekta mbalimbali za umma na binafsi likilenga kuimarisha weledi na kuendana na mabadiliko ya teknolojia katika mifumo ya ununuzi na ugavi.