PSPTB YASISITIZWA KUWACHUKULIA HATUA WANAOKIUKA SHERIA SEKTA YA UNUNUZI
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Musham Ali Munde, ameitaka Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) kufanya ukaguzi wa kina katika taasisi za umma na binafsi na kuwachukulia hatua watumishi watakaobainika kufanya kazi za ununuzi na ugavi bila kufuata sheria.
Ametoa agizo hilo Desemba 19, 2025, jijini Arusha katika ufunguzi wa Kongamano la 16 la Mwaka la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi, linalofanyika kwa siku tatu katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), ambapo alimuwakilisha Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar.
Amesema waajiri wote wanapaswa kuwatumia wataalam wa ununuzi waliothibitishwa na kusajiliwa na PSPTB kwa mujibu wa sheria ili kuimarisha uwajibikaji na ufanisi kazini.
Aidha, amewaelekeza Makatibu Wakuu wa Wizara ya Fedha na OR-TAMISEMI, pamoja na taasisi za PSPTB na PPRA, kushughulikia suala la kuhakikisha wataalam wanaohusika na ununuzi wawe ni wale wenye sifa za kada hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya PSPTB, Jakob Kibona, amesema bodi imeboresha huduma zake kwa njia ya mtandao, ikiwemo usajili wa wataalam na watahiniwa wa mitihani, hali iliyosaidia kuokoa muda na gharama.
Ameongeza kuwa mwaka wa fedha 2024/2025, PSPTB imewajengea uwezo wataalam 3,164 kutoka taasisi za umma na binafsi.