JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi

PSPTB YATAKA TAALUMA YA UNUNUZI IONGEZE IMANI KWA WANANCHI
06 Aug, 2026
PSPTB YATAKA TAALUMA YA UNUNUZI IONGEZE IMANI KWA WANANCHI

Mkurugenzi wa Usajili wa Wanachama na Ushauri wa Kitaalamu kutoka  Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi Tanzania (PSPTB), Amos Kazinza, amesema  kuzingatia weledi, uadilifu na maadili ya taaluma kwa wataalamu wa ununuzi na ugavi ni nguzo muhimu katika kuimarisha usimamizi wa fedha za umma na kuongeza imani ya wananchi katika matumizi ya rasilimali za Serikali.

Kazinza aliyasema hayo jijini Arusha wakati wa Kongamano la Wadau wa Ununuzi wa Umma lililowakutanisha wataalamu wa ununuzi na ugavi kutoka taasisi za Umma na binafsi pamoja na wadau wengine wa sekta hiyo ambalo limeandaliwa na

Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA),kwa lengo la kujadili masuala yanayohusu ununuzi wa Umma na kubadilishana uzoefu wa kuboresha utendaji.

Alisema PSPTB, ikiwa ndiyo mdhibiti wa taaluma ya ununuzi na ugavi nchini, ina jukumu la kusajili wataalamu, kusimamia mwenendo na maadili yao pamoja na kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia viwango vya taaluma.

Katika kongamano hilo, PSPTB iliwasilisha mada kuhusu weledi na uadilifu katika taaluma ya ununuzi na ugavi, ambapo ilisisitiza kuwa misingi hiyo ni muhimu katika kuongeza uwajibikaji, uwazi na ufanisi katika mfumo wa ununuzi wa umma.

Kwa mujibu wa Kazinza, mada hiyo imeandaliwa kufuatia hoja zilizobainishwa katika taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), pamoja na PPRA, ambazo zilionesha kuwepo kwa mapungufu katika baadhi ya maeneo ya usimamizi wa ununuzi wa umma.

Alieleza kuwa kufuatia maelekezo ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya kuwajengea uwezo wataalamu wanaobainika kuwa na mapungufu badala ya kuwataja hadharani ambapo PSPTB imeendelea kutoa elimu na kusisitiza uzingatiaji wa maadili, sheria na kanuni za taaluma hiyo.

"Tunawahimiza wataalamu wetu kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na umahiri wa hali ya juu ili kuhakikisha fedha za walipa kodi zinatumika kwa ufanisi na kwa manufaa ya wananchi," alisema Kazinza.

Aliongeza kuwa PSPTB ina lenga kuona taarifa zijazo za ukaguzi zikionesha maboresho makubwa kwa kupungua kwa hoja zinazohusiana na ukiukwaji wa taratibu za ununuzi wa umma.

Aidha, alisema usimamizi madhubuti wa taaluma ya ununuzi na ugavi utasaidia kuongeza uwazi, uwajibikaji na thamani ya fedha katika utekelezaji wa miradi na utoaji wa huduma za Umma, hatua ambayo itaendelea kujenga imani ya wananchi kwa taasisi zinazosimamia matumizi ya fedha za Serikali.

slot gacor