PSPTB YANG'ARA TUZO TAASISI ZA SERIKALI
BODI ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), imepata tuzo ya mshindi wa pili katika Kundi la Taasisi za Serikali zilizoshiriki Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es salaam (DITF).
Ushindi huo ni kutambua mchango wa bodi hiyo katika kutekeleza majukumu yake ya msingi kwa weledi na ubunifu mkubwa.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano kwa Umma na Mawasiliano wa PSPTB,Shamim Mdee, alisema ushindi huo umetokana na maandalizi ya kina yaliyolenga kutoa huduma bora na zenye tija kwa wageni waliotembelea banda la PSPTB wakati wa maonesho hayo.
“Siri ya mafanikio haya ni maandalizi mazuri na timu yenye ari kubwa ya kuhakikisha kila mgeni anapata huduma bora. Tulihakikisha tunawasikiliza wageni kwa makini, kujibu maswali yao kwa kina na kuwaeleza kwa ufasaha huduma na bidhaa tunazotoa,” amesema Mdee.
Ameongeza kuwa nidhamu ya utumishi wa umma, ubunifu wa banda, na mwonekano wa kuvutia vilichangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha ushindi huo.
“Banda letu lilikuwa la kipekee kwa sababu tuliweka mkazo katika ubunifu, tulionyesha namna rahisi ya kupata huduma zetu kupitia mfumo wa mtandao wa Online Registration System, jambo lililowavutia wageni wengi,” amefafanua.
Mdee amesema ushindani katika kundi la taasisi za serikali ulikuwa mkubwa kutokana na idadi ya taasisi zilizoshiriki, lakini mafanikio hayo ni matokeo ya ushirikiano mzuri na ufanisi wa timu nzima ya PSPTB iliyoshiriki kutoa huduma katika maonesho hayo.
Aidha, ameahidi kuwa PSPTB itaendelea kuboresha huduma zake kwa wadau wa taaluma ya ununuzi na ugavi nchini, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya bodi hiyo katika kukuza weledi, uwajibikaji na ubunifu katika sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) ni chombo cha kitaifa kinachohusika na kusimamia taaluma ya ununuzi na ugavi nchini.
Baadhi ya majukumu yake ni pamoja na kuendesha mafunzo na mitihani ya kitaaluma, kusajili na kusimamia mienendo na maadili ya wataalam wa ununuzi na ugavi, pamoja na kutoa ushauri kwa serikali na sekta binafsi kuhusu masuala ya kitaaluma katika sekta hiyo.
Tuzo hiyo inaonesha jinsi PSPTB inavyoendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuimarisha taswira chanya ya taasisi hiyo katika kukuza taaluma ya ununuzi na ugavi nchini.