JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi

PSPTB YATANGAZA MATOKEO YA MITIHANI YA BODI, YAONYA UDANGANYIFU
22 Jun, 2025
PSPTB YATANGAZA MATOKEO YA MITIHANI YA BODI, YAONYA UDANGANYIFU

 

BODI ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), imetangaza matokeo ya mitihani ya 31 ya bodi hiyo yanayoonesha jumla ya watahiniwa 186 kati ya 382 waliofanya mitihani hiyo wamefaulu sawa na asilimia 50.3.

Mkurugenzi Mkuu wa PSPTB, Godfred Mbanyi, ametangaza matokeo ya hayo na kusema kati ya walioshiriki, 192 (sawa na 50.3%) wamefaulu, 186 (sawa na 48.7%) wamerudia masomo na watahiniwa wanne wamefeli na kulazimika kuanza upya katika ngazi husika.

‎Aidha, ametoa wito kwa watahiniwa waliokosa alama za kutosha kuwawezesha kufaulu wajisajili ili kurudia masomo kwenye mitihani ya Novemba mwaka huu 2025.

Mbanyi amesema dirisha la usajili limefunguliwa na kuwataka wanafunzi waliomaliza vyuo kujisajili kwa ajili ya kufanya mitihani hiyo ya kitaaluma ili waweze kupata sifa stahiki za kitaaluma.

“Wale waliokosa alama za kutosha dirisha la usajili la Novemba 2025 limefunguliwa, tunawahimiza wanafunzi waliomaliza vyuo kujisajili ili kupata sifa stahiki za kitaaluma” amesema, Mbanyi.

‎Sambamba na hilo, amewaonya watahiniwa kuepuka vitendo vya udanganyifu na ukiukwaji wa kanuni za mitihani, akisisitiza kuwa bodi haitasita kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayebainika kufanya udanganyifu.

Amesema adhabu kwa watakaobaikina kufanya udanganyifu kwa mujibu wa kanuni ni pamoja na kufutiwa matokeo ya mitihani yote, kusimamishwa mihula mitatu ya mitihani na kupewa adhabu ya kulipa fedha au kifungo jela.

“Bodi haitasita kuchukua hatua kali zaidi kwa yeyote atakayekiuka maadili ya mitihani, tunahitaji taaluma hii kuheshimika na kuaminika nkwa maslahi ya taifa”, amesema Mbanyi.